June 01, 2009

OPEL KUPIGWA JEKI

Kamati za bajeti katika majimbo mawili ya Ujerumani zimeidhinisha fedha zitakazotolewa kama mkopo kwa kampuni ya magari ya Opel. Uamuzi huo umepitishwa siku moja baada ya makubaliano kufikiwa kuikoa kampuni hiyo ya magari ya Ujerumani kutokana na matatizo yanaoikabili kampuni mama ya Marekani, General Motors, inayokaribia kuwa muflis.

Serikali ya Ujerumani imeahidi kutoa euro bilioni 1.5 kama sehemu ya makubaliano ambapo kampuni ya kuuza vipuri vya magari ya Magna itasimamia shughuli za tawi la kampuni ya General Motors barani Ulaya. Nusu ya fedha hizo zitatolewa na serikali ya mjini Berlin na nusu nyingine zitatolewa na majimbo manne ambako kampuni ya Opel ina viwanda vyake na ambako wafanyakazi takriban 26,000 wanajipatia riziki zao.

Majimbo ya Hesse na North Rhine-Westphalia yameidhinisha sehemu yao ya fedha inayojumulisha euro milioni 600.

Mkopo huo utatumika kugharamia shughuli za kampuni ya Opel mpaka mkataba rasmi kati ya kampuni ya Magna na General Motors utakaposainiwa, jambo ambalo huenda likachukua miezi kadhaa.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22