June 12, 2009

WHO yatangaza homa ya mafua ya nguruwe kuwa janga

Shirika la afya duniani limetangaza rasmi kwamba homa ya mafua ya nguruwe ni janga la ulimwengu mzima.Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Dr Margaret Chan ametangaza uamuzi huo katika kikao cha dharura cha shirika hilo la Umoja wa mataifa mjini Geneva.Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 40 kwa maradhi hayo kutangazwa kuwa janga la dunia.Tangazo hilo limetolewa wakati ambapo visa vya kuenea kwa virusi vya maradhi hiyo vimeongezeka na pia kugunduliwa ushahidi katika eneo la Asia ,Ulaya na hata Amerika kwamba virusi vya homa hiyo vinaambukiza miongoni mwa binadamu.Hata hivyo Dr Chan ametilia mkazo kwamba hali hiyo haina maana kwamba idadi ya vifo kutokana na mkurupuko wa homa hiyo itaongezeka kwa kasi.Hii ni kutokana na kwamba ueneaji wa homa hiyo unaonekana kuwa wa kasi ya wastani.Kwa upande mwingine amezitolea mwito serikali kuongeza juhudi zao katika kukabiliana na homa hiyo lakini amependekeza kutowekwa kwa vikwazo vya usafiri. Shughuli ya kutafuta chanjo dhidi ya Homa ya mafua ya nguruwe inaendelea ingawa chanjo hiyo haitokuwa tayari kabla ya mwezi wa Septemba.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22