September 19, 2009

JAHAZI KUIBUKA NA MPYA SIKU YA EID

MZEE YUSSUF

Kundi la mipasho la Jahazi Modern Taarab `Wazee wa Naksh Naksh' Idd Mosi wanatarajia kutambulisha vibao vyao vipya katika onyesho lao katika ukumbi wa nyumbani wa Travertine Magomeni jijini Dar es Salaam.

Jahazi linaloongozwa na muimbaji nguli Mfalme Mzee Yussuf limekuwa likivuma sana licha ya kutokuwa na muda mrefu tangu lianzishwe na waimbaji wengi waliojiengua kutoka Zanzibar Stars ambalo sasa limepungua makali yake tangu liondokewe na baadhi ya wasanii wake.

Yussuf alithibitisha kuwa Idd Mosi kundi lake litavinjari Magomeni na aliwataka wapenzi kujitokeza kwa wingi kushuhudia kile walichoandaliwa maalum kwa ajili ya siku kuu ya Idd El Fitry.

Kwa sasa Jahazi linaelea katika bahari ya muziki wa mwambao na vibao vyake kama Two in One, Tupendane Wabaya Waulizane, Niepushie, Mkuki kwa Nguruwe, Hayanifiki na Sichoki Kustahimili, ambavyo vimekuwa gumzo kila kundi hilo linapotumbuiza katika kumbi mbalimbali hapa nchini.

Mzee alivitaja baadhi ya vibao hivyo kuwa ni Domo Kaya, Adui Muombee Dua na Kesho Anajua Mungu, ikiwa ni maandalizi yao ya kufyatua albamu mpya ya tano.

Kundi hilo lililoanzishwa mwaka 2006, mpaka sasa limeshatoa albamu nne tofauti, ikiwemo Two In One, Kazi ya Mungu Haingiliwi, Tupendane Wabaya Waulizane na ile ya inayotamba sasa ya VIP.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22