July 22, 2012

UTALII WA MICHEZO” - IBF YAKUSUDIA KUITANGAZA TANZANIA‏

Itatumia mapambano yake kutangaza vivutio vya kitalii vya Tanzania
■ Kila bondia atakayegombea taji lake atavaa nembo zenye vivutio vya kitalii vya Tanzania
Katika hali inayoashiria uzalendo wa hali ya juu, Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi (IBF) litaanza kuvitangaza vivutio vya kitalii vya Tanzania katika mapambano yake yote ya ngumi ili viweze kujulikana zaidi ulimwengumi.
Katika program yake ya “Utalii wa Michezo” iliyowakilishwa na Rais wa shirikisho hilo katika bara la Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi Mtanzania Onesmo Ngowi, na kukubaliwa na mkutano mkuu wa 29 wa Shirikisho la Ngumi la Kimataifa na Chama Cha Ngumi Cha Marekani (IBF/USBA) uliomalizika hivi punde jijini Honolulu, Hawaii programu ya "Utalii ya Michezo ya IBF" imegawanyika katika sehemu tatu:
1.Utalii wa Mikutano ya IBF
2.Utalii wa Kupanda Mlima Kilimanjaro kila mwaka (IBF Mount Kilimanjaro Climb Expedition)
3.Utalii wa mapambano ya Ngumi
Ni katika “Utalii wa mapambano ya Ngumi” ambako shirikisho hili limeamua kuvitangaza vivutio vya kitalii vya Tanzania.
Hii ni mara ya kwanza kwa taasisi ya michezo hapa nchini na katika bara la Afrika kutumia mitandao yake kutangaza vivutio vya kitalii vya nchi ya Afrika.
Akitangaza nia ya IBF kuitangaza Tanzania duniani kote Rais wa shirikisho hilo katika bara la Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi Onesmo Ngowi alisema kwamba ni muhimu sisi Watanzania tuliopewa nafasi katika taasisi za kimataifa tukatambua kuwa nchi yetu inatakiwa kutangazwa.
Kwa kuanzia kila bondia wa Kitanzania atakayewakilisha nchi hii na taarifa yake kuandikwa, taarifa hii itaanza na neo "MTANZANIA" halafu jina lake. Hii ni kuiweka nchi yetu mbele ya kila kitu na hii "BRANDING" kama inavyojulikana katika ulimwengu wa masoko na promosheni za biashara.
Katika mkakati huu MTANZANIA Ngowi alisema kuwa kwa sasa kuna mapambano kadhaa mbayo mabondia wa Kiafrika wanashiriki na watayatumia kutangaza vivutio cya kitanzania. Alisema kuwa bondia Helen Joseph wa Nigeria anayeishi Ghana atapambana na bondia Dahianna Santana wa nchi ya Dominican Repubic na Helen ataitangaza Tanzania.
Mpambano huo utafanyika nchini katika jiji la Santo Domingo nchini Dominican Republic, iliyoko katika eneo la Karibian karibu na Jamaica
tarehe 12 August mwaka huu.
Aidha MTANZANIA Ramadhani Shauri atapambana na bondia Sande Kizito wa Uganda katika mpambano uliopewa jina la “The Rumble in the City” (Rurumai katika jiji) mpambano huo utafanyika siku ya Idd pili katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini dar-Es-Salaam
Naye MTANZANIA Nasibu Ramadhani atapimana ubavu na bondia Twalib Mubiru wa Kenya kugombea mkanda wa IBF Afrika ya Mashariki na Kati katika uzito mwepesi (lightweight) siku hiyo hiyo ya Idd pili, jijini dar-Es-Salaam.
Aidha, MTANZANIA Rajabu Maoja anayeishi katika jiji la Tanga atapimana ubavu na bondia Gottlieb Ndokosho bingwa wa ngumi nchini Namibia kugombea mkanda wa IBF wa mabara katika uzito wa Unyoya. Mapambamo huo uliopewa jina la “The battle of the Kalahari Desert” (Vita vya Jangwa la Kalahari) utafanyika katika jiji la Windhoek nchini Namibia.
Naye MTANZANIA Allen Kamote atapimana ubavu na bondia Wilson Masamba wa Malawi katika mpambano wa kugombea mkanda wa IBF katika bara la Afrika uzito mwepesi "Lightweight" jijini Arusha tarehe 27 Octoba mwaka huu katika mpambano uliipewa jina la "TANZANITE Title" (Ubingwa wa Tanzanite). Mpambano huo utafanyika katika jiji la Arusha na utaandaliwa na bondia wa zamani wa taifa George Andrew.

No comments: