July 22, 2012

Norway yakumbuka mauaji ya kinyama

Wananchi wa Norway wamekusanyika katika makao makuu ya serikali mjini Oslo Jumapili (22.07.2012) kwa ajili ya kumbukumbu ya watu 77 waliouliwa na Anders Breivik katika shambulio la bomu na risasi mwaka mmoja uliopita.
Waziri Mkuu Jens Stoltenberg ameuambia umati uliokusanyika kwenye kumbukumbu hiyo kwamba "Bombu na risasi hizo zilikuwa zimekusudia kuibadili Norway.Wananchi walijibu kwa kufumbata maadili yetu.Muuaji huyo ameshindwa na wananchi ndio walioshinda".
Breivik ambaye alisema wahanga wake ambao takriban wote walikuwa vijana wadogo walikuwa wasaliti kwa sababu waliunga mkono mchanganyiko wa utamaduni na uhamiaji wa Waislamu,aliripua bomu nje ya bunge na kuuwa watu wanane.
Kisha akawauwa kwa kuwapiga risasi watu wengine 69 katika kambi ya vijana ya chama tawala cha Labour katika kisiwa cha Utoeya.

Ni vigumu kusahau

Vegard Groeslie Wennesland muhanga wa mauaji ya Utoeya amesema "Ni watu wachache wanaweza kupitisha siku bila ya kufikiria yale yaliotokea tarahe 22 mwezi wa Julai"
Anasema aidha utakuwa unamjuwa mtu fulani ambaye sasa hayuko tena,rafiki, mshauri au kitu fulani ambacho kinakukumbusha yale yaliotokea.
Mbali na kumbukumbu nyengine katika kisiwa cha Utoeya hapo Jumapili takriban wahanga 1,000 walikutana kwa siri mbali na macho ya vyombo vya habari kwa ajili ya kumkumbu hiyo ambayo ilijumuisha kuachiliwa hewani kwa bofu lenye umbo la kopa waliambatanisha katika kibofu hicho ujumbe wao binafsi.
Wennesland ambaye alinusurika kwa kujifungia ndani ya chumba yeye na wenzake 50 anasema tukio hilo limembadili na hivi sasa amekuwa akiyafurahia maisha hapa na pale.
Kusahao ilikuwa ni vigumu wakati kesi ya wiki kumi ya mmuaji Breivik mwaka huu ilipoamsha kumbukumbu za kutisha kwa ufasaha siku hadi siku.Hukumu inatarajiwa kutolewa tarehe 24 mwezi wa Augusti na repoti ya tume kuhusu matukio hayo inatarajiwa kutolewa wiki zijazo.
Breivik aidha anakabiliwa kuwa chini ya matunzo ya ugonjwa wa akili katika maisha yake yote au kifungo cha miaka 21 gerezani na uwezekano kwa kifungo hicho kurefushwa kwa muda usiojulikana.
Muuaji huyo ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 33 amesema amefayna mashambulizi hayo ili kuilinda nchi yake dhidi ya uvamizi wa Uislamu na amekilenga chama cha Labour kutokana na sera zake za uhamiaji na kuunga mkono kuwepo kwa jamii ya tamaduni tafauti.

Jamii ya wazi

Mashambulio hayo yalilifadhaisha taifa la Norway lenye wakaazi milioni tano ambalo linajivunia kwa kuwa jamii ilio wazi,yenye kupigania muafaka ya kisiasa na yenye mafanikio ya kiuchumi.
Norway imeyakinisha kujizatiti kwake kuwa jamii ilio wazi kufuatia mashambulizi hayo na imekataa wito wa kuchukua misimamo mikali.
Profesa wa elimu ya jamii Thomas Hylland -Erkisen katika Chuo Kikuu cha Oslo anafikri wanasiasa halikadhalika na wananchi pengine bila ya hata kutamka wameweka wazi kwamba wanataka jamii ya Norway iendelee kubakia kama ilivyo.
Amesema watakienzi kile wanachokiona kuwa ni cha thamani kabisa nchini Norway : kuwa wazi kwake na hisia ya usalama.
Katika misa maalum kwenye Kanisa la Oslo Askofu Mkuu Helga Haugland Byfuglien amewaambia Wanorway mwanga huangaza kizani na kwamba kiza hakikuwafudikiza.

Je muuaji alikuwa na akili timamu?

Waendesha mashtaka walitaka mahakama imtangaze Breivik kuwa mwendawazimu kinyume na maoni ya wananchi kwamba ushahidi wake wa akili timamu umeonyesha kuwa anastahiuki kifungo gerezani.Yeye mwenyewe Breivik anataka atangazwe kuwa ana akili timamu na ahesabiwe kuwa mwanaharakati wa kisiasa.
Breivik amesema wahanga wake ambapo mdogo kabisa alikuwa na umri wa miaka 14 walikuwa wameleweshwa tamaduni za Kimaxist ambapo sera zake za uhamiaji zinachafuwa damu safi ya Wanorway na kuhatarisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na Waislamu.
Aliwasili katika kambi hiyo kisiwani Utoeya akiwa amevalia sare ya polisi na kudai kwamba amekwenda kuilinda kambi hiyo kabla ya kuwafyetulia ovyo risasi watoto.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22