Urusi inataka ufafanuzi kutoka kwa serikali ya Uturuki baada ya taifa hilo kulazimisha kutua ndege moja ya abiria ya Syria iliyokuwa ikitoka Urusi kwenda Syria ikiwa na raia kadhaa wa Urusi ndani yake.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imesema serikali ya Uturiki imeshindwa kuwaruhusu wanadiplomosia wao kwenda kuonana na abiria 17 wa kirusi waliokuwemo katika ndege hiyo katika muda wa masaa manane wakati ndege hiyo ikiwa inashikiliwa kutokana na kushukiwa kubeba zana za kijeshi.
Katika kauli yake hiyo Urusi imesisitiza kutaka ufafanuzi wa kitendo hicho kwa kusema kwamba uhai na usalama wa abiria hao ulikuwa katika kitisho kikubwa.
Kiasi fulani cha mizigo kilochokuwa katika ndege hiyo aina ya Airbus A-320 ikiwa na abiria 30, imechukuliwa na serikali ya Uturuki ambapo baadaye iliruhusiwa kuendelea na safari yake.
Ushirikiano wa Urusi na Syria
Urusi ni mshirika mkubwa wa rais wa Syria, Bashar al Assad, ambayo ilizuia maazimio matatu ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ya kuongeza shinikizo dhidi ya utawala huo, huku ikifahamika kwamba iliiuzia serikali ya Assad silaha za karibu kiasi cha dola bilioni 1 mwaka uliopita. Hata hivyo vyanzo vya kijeshi nchini Urusi vinasema taifa hilo bado halijasimamisha kupeleka silaha Syria.
Nchini Syria kwenyewe waziri wa usafirishaji wa Syria ameituhumu Uturiki kwa kufanya kile alichokiita "uharamia wa angani" baada ya wapiganaji wa Kituruki kulazimisha kutua kwa ndege yake ya abiria iliyokuwa safarini kutoka Urusi kwenda Damascus. Kituo kimoja cha televisheni cha Lebanon, kimemnukuu waziri Mahoumud Said akisema hatua hiyo inatatiza mkataba ya huduma za usafari wa anga.
Mapambano yanaendelea
Katika maeneo ya vita idadi kubwa ya watu wameuwawa katika mapigano kati ya jeshi la Syria na waasi. Kwa mujibu wa Shirika la Uangalizi wa haki za binadamu la Syria ndege za kivita zimevurumisha makombora katika eneo la waasi la mji wa kati wa Homs.
Shirika hilo la uangalizi linasema kuwa kati ya watu 69 waliuwawa wakiwemo raia 15 , wanajeshi 21 na waasi 33. Idadi hiyo ya vifo imetokea katika jimbo la Idlib, Damascus pamoja na mji wa kibiashara wa Aleppo.
Mapema leo asubuhi jeshi la Syria limeanzisha upya mashambulizi yake katika eneo la Maaret al-Numan ambalo linadhibitiwa na waasi baada ya mapigano makali yaliyodumu kwa takribani kipindi cha masaa 48. Tangu katikati ya mwezi Julai mwaka huu jeshi la Syria limekuwa katika jitihada kubwa ya kuirejesha katika udhibiti wake baadhi ya miji ili kuweza kuwepo na uwezekano wa kutumia barabara zinazounganisha miji hiyo na mji wa Aleppo.
Source:Dw
No comments:
Post a Comment