Homa ya uchaguzi nchini Ujerumani inazidi, huku uchaguzi wa mikoa ukitarajiwa kufanyika katika mikoa mitatu ya Ujerumani Jumapili ijayo. Mgombea wa chama cha Christian Democratic Unioni, CDU, katika jimbo la Thuringia, Zeca Schall, ambaye ni mzaliwa wa Angola, analindwa na polisi kufuatia vitisho vilivyotolewa dhidi yake na chama cha kihafidhina cha National Democratic, NDP.
Picha za mgombea wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, katika jimbo la Thuringia, Zeca Schall, zimekuwa zikionekana kwenye mabango katika mkoa huo wa mashariki mwa Ujerumani. Picha ya Zeca ambaye ni mzaliwa wa Angola, akiwa katikati ya Wajerumani weupe inadhihirisha kwamba sasa jamii ya Ujerumani imechanganyika na wageni.
Lakini kuna upinzani kutoka kwa baadhi ya Wajerumani. Chama cha National Democratic Party, NPD, hapa Ujerumani kimekataa kata kata kumkubali Zeca Schall, raia wa Angola, asigombee katika uchaguzi wa mkoa wa Thuringia Jumapili ijayo. Chama hicho kimemtaka Zeca arudi kwao, hatua ambayo imezusha hisia mbalimbali kote nchini Ujerumani na kufanya mwanasiasa huyo kuwekewa ulinzi wa polisi.
Tangu mwaka wa 1993, Andreas Minschke, amekuwa akiandaa kampeni za uchaguzi za chama cha Christian Democratic Union, CDU, katika jimbo la Thuringia, lakini bado hajawahi kupata uzoefu wa aina hii. Kwani rafiki yake, Zeca Schall, ambaye alizaliwa nchini Angola na ambaye alihamia hapa Ujerumani miaka 20 iliyopita, amekuwa akipigwa vita na chama cha kihafidhina cha National Democratic Party, NPD. Chama hicho kimekuwa kikimuita Zeca kuwa niga wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, na hivyo kimekuwa kikimtumia kufanya kampeni ya kuwafukuza wageni.
Andreas Minschke anasema, "Kama chama cha NPD kinataka kumhimiza mtu aende nyumbani, huo si mualiko wa chakula cha jioni, bali tayari ni shinikizo. Tumeomba vibali vya kumkamata mtu yeyote atakayemtishia maisha yake na tayari ulinzi wa polisi upo kwa ajili yake."
Zeca Schall ni mmoja kati ya watu ambao wamekuwa wakisadia katika kampeni za uchaguzi wa mikoa za chama cha Christian Democratic Union, CDU. Amekuwa mtu mashuhuri kutokana na kwamba picha yake imechapishwa kwenye bango kubwa la mgombea wa wadhifa wa juu jimboni humo na ambaye ni waziri mkuu wa jimbo la Thuringia, Dieter Althaus, akiwa katikati ya watu wengine wawili wa Thuringia wenye nyuso za kutabasamu. Zeca Schall pia amekuwa akifanya kazi katika ofisi inayohusika na maswala ya maingiliano ya kijamii katika jimbo hilo la Thuringia.
Tangu mwaka 1988 amekuwa akiishi Hildburghausen, mji mdogo ulioko kusini mwa jimbo la Thuringia. Huko ndiko alikokita mizizi na ni mwanachama huria wa zima-moto mjini humo. Kwa miaka mitano, tangu alipopata uraia wa Ujerumani, Zeca, amekuwa mwanachama wa chama cha Christian Democratic Union, CDU.
Hatua ya chama cha kihafidhina cha National Democratic, NPD, kumshambulia Zeca Schall, inaudhi na haikubaliki, anasema bwana Thomas Müller mbunge cha chama cha CDU kutoka mjini Hildburghausen.
"Hilo ni jambo la kukasirisha sana. Lakini kwa upande mwingine nadhani kwa raia wanaotaka kujifunza kutokana na swala hili, ni ishara ya wazi kabisa vipi chama cha NPD kilivyoghadhabishwa, na natumai kitaadhibiwa katika uchaguzi ujao."
Huku uchaguzi wa mikoa ukitarajiwa kufanyika Jumapili ijayo hapa Ujerumani, wachunguzi wa maswala ya uchaguzi wanaamini kwamba chama cha NPD safari hii hakitaweza kushinda zaidi ya asilimia 5 ya kura. Hii ina maana huenda kisiweze kutuma wajumbe wake katika bunge la mkoa. Na ikiwa ubashiri huo ni kweli, basi chama cha NDP na kampeni yake ya kutaka kuwafukuza wageni hakitakuwa na nafasi katika uchaguzi nchini kote.
Chama cha CDU jimboni Thuringia kimetoa nafasi kwenye tovuti yake katika mtandao wa intaneti ambako watu wanaandika maneno ya kumuunga mkono Zeca Schall na kupuuzilia mbali yanayosemwa na wafuasi wa chama cha NPD.
Mgombea uwaziri mkuu wa jimbo la Thuringia kwa tiketi chama cha Die Linke, Bodo Ramelow, alitaka kumtembelea bwana Zeca Schall ili kumpelekea ujumbe wa kumuunga mkono, lakini chama cha CDU jimboni humo kikakataa. Chama hicho badala yake kimewataka wagombea wa vyama vingine vya kisiasa wasimkaribie Zeca Schall.